Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mkuu wa wilaya ya Arumeru Jerry Muro wamegawa vitambulisho vya wajasiriamali awamu ya pili mkoani humo, ambapo Gambo amemkabidhi DC Muro vitambulisho 10,000 ambavyo vinatakiwa kusambazwa katika Halmashauri mbili za wilaya hiyo.
Katika maelezo yake, Muro amesema kuwa walikamilisha ugawaji wa vitambulisho kwa awamu ya kwanza na kwamba atahakikisha vitambulisho 5,000 vinasambazwa katika kila wilaya kwa awamu ya pili.
“Kama mnavyoona mimi na timu yangu yote tumeingia sokoni na tumefanya kazi mmeona watendaji wangu wa kata wafanyakazi wa Halmashauri wote bila kujali cheo, tumeingia kugawa vitambulisho kwa machinga na tumegawa vitambulisho 1,000 na tunaendelea kugawa katika masoko yote”. Ameeleza Mkuu wa wilaya huyo.
Kwa upande wake, RC Gambo amesema kuwa ameona kuna umuhimu wa kushiriki na kuwapa motisha ya ugawaji wa vitambulisho watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo huku akisisitiza kukamilisha zoezi hilo.