Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amewataka wananchi wa Kata ya Swaswa, Manispaa ya Dodoma kuchangamkia fursa ya ujasiriamali zitakazojitokeza wakati wa ujenzi wa barabara ya Martin Luther kuelekea Swaswa yenye urefu wa kilomita 1.9. Jafo ametoa wito huo wakati akikagua miundombinu ya barabara jijini Dodoma na kuwaagiza Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kukamilisha barabara hiyo katika kipindi cha mwezi moja kuanzia sasa. Aidha Waziri Jafo amesema mradi huo utaleta fursa mbalimbali za utoaji huduma za kijamii na kuwataka wananchi kutumia nafasi hiyo kujipatia kipato.
“Mungu akijalia tarehe 21 mwezi Desemba mwaka huu ntakuwepo hapa site kukagua kama mradi huu umekamilika kwa wakati na upo katika ubora unaohitajika. Nimeridhika na ujenzi wa barabara ya TPS, upo katika hatua mbalimbali na ujenzi unaenda vizuri nimejionea mpaka sasa na wameniambia ujenzi huu upo katika asilimia 20’’. Amesema Jafo.
Kwa upande wake, Mkuu ya wilaya wa Dodoma mjini, Patros Katambi amesema ni jukumu lake kuhakikisha maagizo yote yanayotolewa na viongozi wake wa ngazi za juu yanatekelezwa kwa kushirikiana na viongozi wake wa ngazi ya wilaya.