Kundi kubwa la vijana wameendeelea kuvutiwa kuwa wajasiriamali ili kuleta maendeleo. Kutokana na ugumu wa ajira, wengi wamekuwa wakielekeza nguvu kubwa katika kujiajiri wenyewe na vilevile kuajiri wengine. Changamoto kubwa kwa wanaoanza biashara ni kushindwa kufanya utafiti wa kina kujua ni shughuli ipi hasa wanatakiwa kufanya. Wengine tayari wameanzisha biashara zao lakini wanakwama kutokana na kwamba, hawakutafakari kwa kina na ushindani mkubwa uliopo sokoni umepelekea biashara zao kudorora na nyingine kufungwa kabisa.
Unawezaje kutambua fursa?
Jambo la kwanza ambalo kila mtu anatakiwa kufahamu kabla ya kuwa mjasiriamali ni kwamba ‘mjasiriamali bora ni mjasiriamali ambaye anasuluhisha changamoto zinazomzunguka’. Kwa kufanya hivyo, unawapa watu kitu ambacho hakikuwepo mwanzoni na kuwarahisishia maisha. Hali hii itapelekea kuwa na wateja wa uhakika kwani wanahitaji bidhaa/huduma yako katika maisha yao ya kila siku hivyo biashara yako itadumu kwa muda mrefu.
Namna nyingine ambayo mjasiriamali anaweza kutumia ni kwa kubuni kitu kipya kabisa ambacho hakipo sokoni. Unapotambulisha kitu ambacho watu hawakuwa nacho mwanzoni, biashara inakuwa na uhakika wa kufanya vizuri kutokana na kwamba, watu wanapendelea kwenda na wakati. Wangapi mnakumbuka bidhaa ya nazi kutoka Bakhresa? Bidhaa hii ilifanya vizuri sana sokoni kwa sababu hakukuwa na kitu kama hicho hapo mwanzo. Nazi za Bakhresa zimerahisisha maisha ya watu wengi na hiyo ndio sababu ya mafanikio yake. Fursa kama hizi ndizo ambazo wajasiriamali wanatakiwa kuziangalia na kuzichangamkia.
Mbinu ya tatu ya kutambua fursa ni kutafuta soko jipya kwa ajili ya bidhaa ambazo tayari zipo na zinafanya vizuri sokoni. Fikiria jinsi mamia ya watu wanavyoenda sokoni Kariakoo kila siku kutafuta mahitaji. Sasa jiulize watu hawa wanatumia muda ba gharama kiasi gani kila siku kufika Kariakoo? Kwanini usiwarahisishie kazi? Badala ya kuja mjini kila siku kwanini usipeleke bidhaa hizo maeneo ya karibu zaidi? Mfano mzuri wa biashara ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa mtindo huu ni ukurasa maarufu wa Instagram unaofahamika kama Usiende Kariakoo. Mjasiriamali huyu amefanikiwa kupeleka bidhaa kutoka Kariakoo sehemu mbalimbali zikiwemo eneo la Sinza jijini Dar es salaam na mikoa ya Arusha, Mwanza na Dodoma. Badala ya watu kwenda sokoni, ameamua kusogeza soko karibu zaidi kwa watu tena kwa jumla na rejareja, aliona fursa hii na kuichangamkia.
Kama unafikiria kuwa mjasiriamali, hakikisha unawekeza muda wa kutosha kufahamu soko na wateja wako. Angalia wengine wanafanya nini na tumia nafasi hiyo kuchunguza nini kinakosekana kisha tumia ujuzi huo kufanya maboresho ambayo yatashawishi wateja kuichangamkia biashara yako. Unapogusa maisha ya watu walio wengi katika biashara yako, unakuwa katika nafasi nzuri ya kufanikiwa na kufika mbali. Fedha pekee hazitoshi katika hili, ni muhimu kujua jamii inachohitaji na kufahamu wateja unaowalenga ni watu wa aina gani.