Meneja wa Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) mkoani Ruvuma Martin Chang’a ametangaza mkoa huo kuwa mwenyeji wa maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali kwa mikoa ya ukanda wa nyanda za juu kusini yanayotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Oktoba. Maonyesho hayo yatakayofanyika wilayani Mbinga yatawakutanisha takribani wajasiriamali 400 kutoka ndani na nje ya nchi.
Chang’a ameeleza kuwa, walengwa wakuu wa maonyesho hayo ni wajasiriamali ambao wanatengeneza na kufungasha bidhaa wenyewe, lengo likiwa ni kuwapatia mafunzo, kuwakutanisha na kubadilishana mawazo na vilevile kutoa fursa kwa wajasiriamali hao kujitangaza na kuuza bidhaa zao.
Maonyesho hayo yanatarajia kufika tamati Oktoba 8 na mbali na wajasiriamali kutoka Mbeya, Songwe, Ruvuma, Rukwa na Iringa, wajasiriamali kutoka mikoa mingine wamedhibitisha kuhudhuria. Mbali na wajasiriamali, Chang’a pia amebainisha kuwa SIDO itawakutanisha na taasisi kama TanTrade, TFDA, TBS pamoja na halmashauri na wanatarajia kuanzisha mtandao kwa ajili ya wajasiriamali na wamiliki wa viwanda kutoka kanda ya nyanda za juu kusini.
Kwa mujibu wa maelezo ya Meneja huyo, tayari SIDO mkoa wa Ruvuma wameanza maandalizi kwa ajili ya maonyesho hayo huku sehemu kubwa ya bidhaa zitakazoonyeshwa zikiwa mashine ili kuelimisha na kuhamasisha wananchi kufikiria kuanzisha viwanda vidogo.