Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Masoko ya muda mfupi yachangamkiwe

Masoko ya muda mfupi yachangamkiwe

0 comment 108 views

Masoko ya muda mfupi maarufu kama ‘Pop up Market’ ni masoko ambayo huandaliwa kwa ajili ya wafanyabiashara au wajasiriamali katika maeneo yenye nafasi kubwa ambayo yanawezesha wafanyabiashara kuweka bidhaa zao kwa ajili ya kuwauzia wateja mbalimbali mara nyingi hufanyika siku moja.

Katika masoko haya, mjasiriamali/mfanyabiashara hupata sehemu/meza ya bei nafuu kwa ajili ya kuweka bidhaa zake, hivyo ni rahisi kuwashawishi wengi kutumia fursa hiyo kutokana na unafuu wake.

Waandaji wa masoko hayo ya muda mfupi, hutangaza kuhusu eneo ambalo biashara hizo zitafanyika ili kuhakikisha wajasiriamali wanajipatia wateja wapya. Pia wajasiriamali huwarahisishia wateja wao wa kuzoeleka kwenda kununua bidhaa, kuzungumza na kutoa maoni kuhusu huduma au bidhaa husika.

Masoko ya muda mfupi sio kitu kigeni. Inaelezwa kuwa soko la kwanza liliandaliwa katika soko la Disemba la Vienna mwaka 1298. Hapa kwetu, idadi ya masoko ya muda mfupi ambayo yamefanyika ni machache ingawa watu wanaendelea kujua kuhusu masoko hayo, na kwa upande wa wajasiriamali nao wameanza kuhamasika kwenda kushiriki katika fursa hizo. Kwa mfano kwa sasa wajasiriamali wengi hasa vijana wanapeleka bidhaa zao katika soko la muda mfupi ambalo linafanyika mara moja kwa mwezi maeneo ya Mikocheni-Tips Lounge, Dar es salaam.

Umuhimu:

Sio kila mjasiriamali ana uwezo wa kupanga sehemu ya biashara yake. Hivyo kupitia masoko ya muda mfupi, mjasiriamali/mfanyabiashara hasa yule ambaye hana eneo la biashara anapata fursa ya kuwaonyesha wateja zaidi biashara yake hivyo kujipatia wateja wapya bila kutumia fedha nyingi kwa ajili ya pango. Na kutokana na uhaba wa ajira hasa kwa vijan,a masoko haya yanawafaa sana kwani badala ya kusubiria kuajiriwa kijana anaweza kuanzisha biashara yake hata nyumbani na kutumia fursa kama hizo kupanua wigo, na kupata uzoefu zaidi kutoka kwa wafanyabiashara wenzake.

Soko la muda mfupi humkutanisha mteja na mfanyabiashara. Hali inayopelekea watu hawa wawili kufahamiana zaidi, kwani mteja akijionea kwa macho kitu alichokuwa anakisikia au kuona mitandaoni basi anaweza kutoa maoni yake kuhusu bidhaa husika. Hii humrahisishia mfanyabiashara kujua mapungufu yake, wapi anafanya mambo sahihi na kitu gani aboreshe ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora.

Kupitia masoko haya, licha ya kujipatia fedha mfanyabiashara hupata elimu kutoka kwa wafanyabiashara wengine, kwa macho (kuangalia watu wengine wanavyofanya) na hata kwa kuuliza. Kwa sababu masoko haya hulenga kuwakutanisha wajasiriamali wa aina mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi.

Ingefaa kwa waandaaji wa masoko haya kufanya utafiti wa kutosha kuhusu maeneo ya kuweka shughuli hiyo ili kuhakikisha wajasiriamali wanapata wateja wa kutosha. Pia kutumia mifumo mbalimbali ya usambazaji wa habari ni muhimu ili kuhakikisha watu (wajasiriamali na wateja) wa rika zote wanapata habari kuhusu shughuli hiyo.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter