Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Mchakato wa vitambulisho vya wajasiriamali umefanikiwa?

Mchakato wa vitambulisho vya wajasiriamali umefanikiwa?

0 comment 164 views

Kwa miaka mingi wafanyabiashara nchini hasa wajasiriamali wadogo wamekuwa wakilalamikia tozo kubwa za kodi katika maeneo yao ya biashara, hali ambayo imepelekea wafanyabiashara wengi kufunga biashara zao, kutokana na kushindwa kumudu tozo hizo. Mwaka 2016, Rais Magufuli aliamuru machinga wasisumbuliwe, lakini tamko hilo halikutiliwa maanani kama ilivyotakiwa Wajasiliamali hao waliendelea kusumbuliwa kuhusiana na maeneo, na zaidi ya yote tozo kubwa za kodi katika biashara zao ziliendelea.

Desemba 10 mwaka jana, Rais Magufuli  alizindua vitambulisho 670,000 maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na kuagiza wakuu wa mikoa na wilaya  zote Tanzania Bara kuvigawa ili kuboresha mazingira ya kazi ya sekta hiyo.

Lengo la kuanzisha vitambulisho hivyo ilikuwa ni kumsaidia mjasiriamali anayeingiza fedha chini ya shilingi milioni 4 kwa mwaka na kutangaza gharama ya vitambulisho hivyo kuwa ni Sh. 20,000 tu kila mwaka kwenda Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na kutosumbuliwa tena na taasisi hiyo hadi mwaka utakapoisha.

Rais Magufuli alikuwa na nia njema wakati anaanzisha vitambulisho hivi, lakini swali linakuja je, ni wamachinga wangapi wataweza kumudu tozo hiyo ya Sh. 20,000 kila mwaka ili hali mitaji ya wamachinga wengi ni chini ya laki moja?

Ni vizuri kama utafiti ungefanywa ili kukabiliana na changamoto ambazo zinaweza kusababisha vitambulisho hivyo visiwakomboe wamachinga nchini katika suala zima la tozo za kodi. Hata baada ya uzinduzi wa vitambulisho hivi, baadhi ya wamachinga wameendelea kutoa malalamiko kuwa bado wanaendelea kudaiwa kodi kila siku na kuomba Rais kuwapunguzia gharama hiyo.

Pia suala la vitambulisho hivyo kutokuwa na picha inayomuonyesha mmiliki nayo inaweza kuleta shida hapo baadae kwa sababu wakati wa ukaguzi kitambulisho kimoja kinaweza kutumiwa na wamachinga wengi katika maeneo tofauti kutokana na baadhi yao kutokuwa na uwezo wa kuwa nacho.

Wakuu wa wilaya na mikoa wanaendelea kugawa vitambulisho hivyo, na hivi karibuni Rais Magufuli ameeleza katika moja ya hotuba zake kuwa bado hajapata ripoti yeyote kutoka kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo, hivyo inakuwa ngumu kujua hadi sasa ni fedha kiasi gani zimeshapelekwa TRA na wakuu wa wilaya na mikoa wapi hawataki kutekeleza agizo hilo ili aweze kuwachukulia hatua.

Japokuwa idadi kubwa ya wafanyabiashara wamempongeza Rais Magufuli na kupokea vitambulisho hivi kwa mikono miwili, inapaswa kufahamu mafanikio na changamoto ya vitambulisho baada ya zoezi la ugawaji kukamilika. Hii itasaidia kuelewa wapi pafanyiwe marekebisho na wapi paboreshwe zaidi kwani lengo ni kuleta unafuu kwa wajasiriamali na kuhakikisha wananufaika na biashara zao na vilevile kuchangia katika pato la taifa.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter