Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Nyuki wanavyoweza kukupa utajiri

Nyuki wanavyoweza kukupa utajiri

0 comment 188 views

Wazo la kwanza ambalo watu wengi hupata wakisikia nyuki ni hatari kwa sababu ya tabia yao ya kuuma. Licha ya kufanya hivyo, nyuki wanatengeneza vitu vingi ambavyo vina faida na vikiuzwa vinaweza kuleta utajiri mkubwa. Watu hufuga nyuki kwa njia za asili na njia za kisasa. Kufuga nyuki kwa njia za asili huchukua muda kupata matokeo kuliko kufuga nyuki kwa njia za kisasa hivyo ikiwa unataka kufuga nyuki jitahidi kuelewa njia zote ili kufanya maamuzi sahihi.

Ufugaji nyuki una faida mbalimbali zikiwemo:

Asali

Hii ni moja ya bidhaa ambazo hutokana na nyuki na kupitia asali watu mbalimbali wametajirika. Inaelezwa kuwa kwa barani Afrika watu wanatumia asali mara tatu zaidi ya ile inayozalishwa hivyo watu wanatakiwa kuchangamkia fursa ya uzalishaji wa asali kwa sababu kuna soko la uhakika. Watu hufurahia kutumia asali kwa sababu imeshathibitishwa kuwa inaweza kutumika kama dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali, vilevile inaweza kutumika katika chakula na uwekaji wa asali katika vitu husababisha vitu hivyo visiharibike ndio maana watu wengi huona umuhimu wa kununua asali kwa kuwa inaweza kutumika katika mambo mengi kwa mara moja. Hivyo ili kujipatia soko, unatakiwa kuwa makini na vifungashio vyako ili kuwavutia watu wa ndani na nje ya nchi kununua asali zako.

Nta

Wazalishaji wengi wa nyuki hutupa nta bila kujua faida wanayoweza kuipata kutokana na bidhaa hii. Nta kutumika katika mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na katika viwanda vya usindikaji chakula, hutumika kutengeneza mishumaa, katika vipodozi kama mafuta. Pia hutumika kwenye polishi ya viatu na samani n.k. Uzuri wa nta ni kwamba huwa haiharibiki hivyo kila ukitaka kuitumia unaiyeyusha na kurudia tena hivyo mara nyingine. Hivyo kwa kuuza nta mzalishaji anakuwa na uhakika wa soko katika viwanda na hata kwa watu binafsi.

Sumu ya nyuki (Bee Venom)

Nyuki hutengeneza sumu kwa ajili ya kujikinga na hatari. Lakini kwa upande wa binadamu sumu hiyo hutumika kuponya magonjwa. Hivyo  basi mfugaji nyuki anaweza kuongea na taasisi zinazojihusisha na masuala ya utengenezaji dawa kwa kutumia sumu hiyo na kuingia nao mkataba wa kufanya biashara.

Gundi

Nyuki hutumia gundi yao kurekebisha mizinga yao kwa kuziba sehemu zenye ufa ili wadudu au maji yasiingie ndani. Gundi hiyo hutumika kutibu magonjwa ya fangasi, vidonda vya tumbo, ngozi iliyoungua na hata magonjwa ya mlipuko. Ikiwa mtu amepata matatizo haya lazima ataenda kununua gundi kwa wazalishaji ili kuondokana na magonjwa hayo. Pia katika sekta ya afya lazima wanunue gundi hiyo ili kutengeneza dawa.

Maziwa ya nyuki

Haya hutengenezwa na nyuki vijakazi. Utafiti unaonyesha kuwa maziwa haya yana vitamini b na watu huyatumia kwa ajili ya kupata muonekano wa vijana huku ikielezwa kuwa maziwa haya huongeza nguvu za kiume. Mziwa haya yanatumika sana barani Asia kwa ajili ya dawa. China peke yake hutumia tani 75 kwa mwaka hivyo mfugaji wa nyuki anaweza kuchangamkia fursa hii na kuuza maziwa ya nyuki katika soko la kimataifa.

Watanzania hususani vijana wanatakiwa kuacha uoga kwenye suala la ufugaji wa nyuki na kuchangamkia fursa zilizopo ili kuleta maendeleo. Ni muhimu kusoma zaidi kuhusu ufugaji huu na pia kukutana na afisa maliasili ili kupata elimu zaidi na baadae kuwekeza katika ufugaji huu.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter