Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage leo hii anatarajia kuzindua Tamasha la Mwanamke Mjasiriamali Tanzania (MOWE) linalolenga kutambulisha ubunifu, taaluma na ufundi wa kutengeneza bidhaa za mikono. Tamasha hilo litakalofanyika katika viwanja vya Nyerere jijini Dodoma pia litatumika kama fursa ya kutambulisha bidhaa za wanawake wajasiriamali wapatao 250 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ujumla.
Mwenyekiti wa tamasha hilo Louis Kiluwa ameeleza kuwa tamasha hilo linafanyika mahali hapo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake rasmi mwaka 2006 likiwa na lengo la kuunga mkono uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuhamishia makao makuu ya nchi jijini humo na hivyo kuwapa fursa mbalimbali wananchi. Kiluwa amesema kuwa wameamua kufanya tamasha hilo Dodoma ili kuwapa hamasa wajasiriamali katika mkoa huo.
Tamasha la Mwanamke Mjasiriamali Tanzania limeandaliwa kwa pamoja na wawakilishi wa vikundi takribani 20 vya ujasiriamali pamoja na taasisi za serikali ili kutoa nafasi ya kuonyesha vipaji walivyonavyo wajasiriamali. Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo ni moja kati ya taasisi za serikali zilizoalikwa katika tamasha hilo, Rhoida Andusamile amesema wapo bega kwa bega na wajasiriamali katika kuhakikisha bidhaa zao zinazingatia ubora na viwango.