Wajasiriamali wanaomiliki mashine za kusaga na kukoboa mahindi kutoka maeneo mbalimbali jijini Dar es salaam wamepongeza hatua ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwafuata kuanzia ngazi ya chini na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa unga unaozalishwa kuwa na viwango ili kulinda afya za wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wajasiriamali hao wamesema nia ya Shirika hilo kuwasaidia kuhakikisha kuwa wanazalisha unga ulio na viwango na kuwataka wengine kutosita kuwapa ushirikiano.
“Wenye mashine za kusaga mahindi tusiogpe kutoa ushirikiano kwa sababu Shirika hili linataka kutufikisha juu na hatimaye tukaweza kupata masoko ya nje ya nchi badala ya kutegemea wateja wa ndani peke yao”. Amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa TBS, Baraka Mbajije amesema lengo la Shirika hilo kutoa elimu kwa wazalishaji ni kuhakikisha bidhaa hizo zinakidhi viwango.
“Kwa hiyo mbali na kununua sampuli za unga ili zikapimwe kwenye maabara zetu tunatoa elimu kwa wazalishaji namna bora ya ufungashaji wa bidhaa hiyo”. Ameeleza Mbajije.