Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Valley Mutakyamirwa amesema taasisi hiyo itaendelea kuwajenga uwezo wajasiriamali ili waweze kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili kwa kuweka mikakati ya pamoja baina ya wanachama wake. Mutakyamirwa amesema hayo jijini Dodoma na kuongeza kuwa, TPSF inalenga kuwainua wajasiriamali ili waweze kuongeza uzalishaji na kukuza biashara zao ili nao wachangie katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
“Wajasiriamali hawa ni wanachama wetu hivyo jukumu letu ni kuhakikisha kuwa tunashirikiana nao katika kuibua changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ambayo tunashirikiana na Serikali katika kuona namna bora ya kuzitatua”. Amesema Mkurugenzi huyo.
Mutakyamirwa ameeleza kuwa, serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wajasiriamali ikiwemo kujenga miundombinu, kupunguza VAT kutoka asilimia 20 hadi 18, hatua ambayo amesema inaonyesha dhamira ya dhati ya serikali kuendelea kuimarisha sekta ya ujasiriamali na biashara kwa ujumla.
Warsha ya kuwajengea uwezo wajasiriamali ambao ni wanachama wa taasisi ya TPSF inafanyika kwa muda wa siku mbili jijini Dodoma, lengo kuu likiwa ni kuwajengea uwezo wajasiriamali hao ili waweze kuongeza tija katika shughuli wanazofanya.