Ujasiriamali au kujiajiri sio kazi rahisi kama watu wengi wanavyofikiria. Uvumilivu ni jambo la msingi ikiwa unataka kufanya ujasiriamali, kwa sababu siku zote hakuna mtu anayejua nini kitatokea kesho hivyo kama mjasiriamali unatakiwa kuwa na mipango lakini ni muhimu kujiandaa kwa jambo lolote linaloweza kutokea.
Watu wengi wameanzisha biashara na kukata tamaa kipindi biashara hizo zinaposhindwa kufika mbali kama walivyotegemea. Kitu ambacho kila mtu anatakiwa kujua ni kwamba, kushindwa ni jambo la kawaida. Pia kushindwa katika ujasiriamali wa aina moja haimaanishi kuwa huwezi kuanzisha biashara nyingine na ikashindikana pia. Kuna watu wameanzisha biashara kadhaa na kushindwa kuendesha biashara hizo lakini kwa sababu hawakukata tamaa wakaanzisha biashara nyingine na kupata mafanikio.
Ni muhimu kujua kila kitu kina wakati na uhitaji wake na kujua bidhaa au huduma itakayokuletea mafanikio ni muhimu kufanya utafiti wa kina.
Vifuatavyo ni vidokezo vitakavyokusaidia kufanikiwa katika sekta ya ujasiriamali:
Kuwa mwanzilishi hakutakusaidia kuendesha biashara yako ikafikia malengo. Lakini kufanya shughuli ambazo una ujuzi nazo kutasaidia biashara iwe na maisha marefu, kufanya kazi na timu ambayo mnaenda sawa kutaongeza uzalishaji na ufanisi wa kazi hivyo kutimiza malengo. Mambo ambayo wengi huona ni madogo na hayatakiwi kuzingatiwa ndiyo yanayoweza kufikisha mbali biashara.
Jikumbushe kuwa bado una muda. Acha kufikiria kuwa umri umeenda kuanza kujihusisha na biashara kwani siku zote uzoefu ni muhimu. Kama utaepuka madeni ukiwa na miaka 20+ na kuweka akiba zaidi basi ukifikisha miaka 40 utakuwa na hali nzuri ya kukabiliana na hatari mbalimbali za uwekezaji kwa sababu utakuwa umejifunza mambo mengi. Hakikisha hali yako ya kifedha ni nzuri kabla ya kuwekeza katika ujasiriamali.
Unaweza kujihusisha na kampuni mbalimbali kwa kujitolea au kuajiriwa moja kwa moja ili kupata uzoefu ambao utakusaidia pale utakapoanzisha kampuni yako. Kuwa na biashara au kampuni kuna faida lakini wakati huo huo ni rahisi pia kufeli. Ikiwa biashara yako haitafanya vizuri usikate tamaa, jaribu tena na tena.