Hapa Tanzania, asilimia kubwa ya watu hawana ufahamu au uelewa kuhusu masuala ya mirathi na kuandika wosia kabla ya umauti. Suala hili limekuwa geni katika jamii yetu na ni wachache sana wanaofahamu umuhimu wa haya. Wadau wa sheria, haki za binadamu pamoja na mashirika mengine husika wamekuwa hawaweki mkazo katika suala hili kama ilivyo kwa mengine. Lakini bila shaka tumeshuhudia wajane, watoto na ndugu waliofiwa na mpendwa wao wakiteseka mahakamani ili kupata haki zao na kuendesha maisha yao kama ilivyokuwa awali.
Ni wazi kuwa walio wengi wanakosa elimu ya mambo haya jambo ambalo linapelekea migogoro ya kifamilia. Unakuta ndugu wanatumia muda na fedha nyingi mahakamani pale inapotokea wamempoteza mtu ambaye hakubahatika kuandaa wosia hivyo kila mtu anataka mali fulani ili maisha yake yaendelee na asiyumbe kiuchumi. Inawezekana fedha hizi na muda wanaotumia kutafuta haki zao zingeweza kuwekezwa katika harakati nyingine za kimaendeleo na kuwaletea faida.
Jifikirie kama itatokea kesho haupo tena duniani familia yako unaiacha vipi? Wataendelea kuishi katika nyumba yao? Watoto wataendelea na masomo yao? Biashara nazo zitaenda? Kiufupi ni lazima tujiulize mara mbili kuwa hawa utakao waacha nyuma unawaacha vipi? Katika nchi zilizoendelea watu wengi wana uelewa wa mambo ya mirathi na hivyo wengi hujiandaa mapema ili kujihakikishia kuwa hata wasipokuwepo, waliopo hawataachwa katika hali ya sintofahamu.
Hali hapa kwetu ni tofauti. Wengine wanaamini kuwa kuandaa wosia ni kujitakia mabaya, wengine hawaruhusiwi kufanya hivyo kutokana na itikadi za dini au kabila. Mbali na changamoto hizo, ni wazi kuwa elimu haijatolewa vya kutosha katika jambo hili. Tatizo la migogoro katika familia baada ya misiba limekuwa kubwa sana hapa kwetu na kwa kiasi kikubwa linaathiri shughuli nyingine za maendeleo. Watu wanashindwa kuendelea mbele kutokana na kwamba hawajui haki zao, wamekosa elimu stahiki la urithi na pia wanakosa usaidizi wa kisheria kutatua matatizo kama haya.
Migogoro hii imekuwa ikiwazuia wengi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi hivyo ni lazima suala hii litafutiwe suluhisho. Ni lazima jamii ielimishwe na wataalamu wa sheria kuhusu mirathi na haki zao za msingi. Ni lazima tujenge mazoea ya kufuatilia masuala kama haya kwani mara nyingi yanakuwa na madhara makubwa huko mbele.
Wakati wa kuachana na imani potofu ya kuwa kuandika wosia ni kujitabiria kifo umefika. Ni muhimu kwa jamii kujenga utaratibu wa kutayarisha wosia ili kuepusha migogoro ya aina yoyote katika familia. Elimu zaidi iendelee kutolewa ili kuwafahamisha watanzania kuhusu umuhimu wa kuandaa wosia.