Na Mwandishi wetu
Baada ya kufanya mazungumzo na Rais John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) Jose Graziano da Silva amesema kuwa shirika hilo lipo tayari kushirikiana na Tanzania ili kufanya mabadiliko katika sekta ya kilimo. Amesema mabadiliko hayo yatahusisha uzalishaji wa mazao pamoja na viwanda vya uchakataji ili kuongeza thamani ya mazao hayo.
Mkurugenzi huyo pia amemshukuru Rais Magufuli kwa kutoa ushirikiano wake kwa shirika hilo ambalo limekuwepo hapa nchini kwa takribani miaka 40 na kuongeza kuwa kupitia mabadiliko yatakayotokana na kuunganisha sekta ya kilimo na viwanda hasa vya kusindika nyama na samaki, Tanzania inaweza kufaidika na ongezeko la uzalishaji wa chakula, biashara za ndani na nje, ajira pamoja na kuongezeka kwa pato la taifa.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu inasema kuwa Rais Magufuli amemhakikishia Graziano da Silva kuwa serikali yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na shirika hilo huku akisisitizia juu ya dhamira yake ya kutaka ushirikiano huo uelekezwe zaidi katika ujenzi wa viwanda ambavyo vitatumia mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuzalisha bidhaa.
Rais Magufuli pia amesema serikali imejipanga kusimamia miradi yote itakayoletwa hapa nchini ili itekelezwe kwa uadilifu na ubora wa hali ya juu akiongeza kuwa nchi inahitaji wadau kama FAO ili kuzidi kuimarisha uchumi kupitia sekta ya viwanda na kilimo kwani asilimia 75 ya nguvukazi ya taifa ni vijana ambao wana uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao mengi.