Halmashauri za Wilaya nchini zinahamasishwa kuendelea kutenga maeneo kwa ajili ya mashamba ya pamoja (Block Farm) kwa ajili ya kuwezesha vijana kufanya kilimo biashara kupitia Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT).
Wito huo umetolewa na Mhandisi Godwin Makori ambaye anaratibu na kusimamia kazi ya kuhakiki na kupima mashamba kwa ajili ya kuyaandalia hati miliki na kupima afya ya udongo katika maeneo ambayo hali za afya ya udongo hazijulikani.
Kazi hiyo inajumuisha wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, Sekretarieti ya Mkoa, Kamishna wa Ardhi Msaidizi, Halmashauri za Wilaya na Serikali za Vijiji katika mkoa wa Kagera.
Akiwa katika kijiji cha Minazi kata ya Bujugo Halmashauri ya Bukoba Vijijini Mhandisi Makori amesema timu ya wataalam itayafikia maeneo yaliyotengwa na Halmashauri na kuyapima ili kuwezesha upatikanaji wa Hati miliki na kupima afya ya udongo ili vijana watakapoanza kuzalisha katika mashamba hayo wazalishe kwa uhakika kwa kuwa watakuwa wanajua mazao yanayofaa kulimwa kulingana hali ya udongo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Toba Nguvila amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kuwezasha vijana kupitia BBT kwani uzalishaji wa mazao utaongezeka na vijana wa Tanzania watapata ajira.
Ameongeza kuwa Viongozi na wananchi wa mkoa wa Kagera wanaunga mkono jitihada za Wizara ya Kilimo chini ya uongozi wa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwa maslahi mapana ya maendeleo ya mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla.