Wakulima wa mbaazi wana kila sababu ya kucheka baada ya bei ya zao hilo kupanda.
Mwaka jana mbaazi iliuzwa kwa Tsh 300 kwa kilo ambapo imepanda na kufika Tsh 2000 mwaka huu.
Rais Samia Suluhu Hasani amesema hayo akizungumza katika Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Kama mtakumbuka kwa miaka mitatu nyuma tulihamasisha wakulima walime sana mbaazi, wakalima sana mbaazi lakini kwa sababu hatukuwaunganisha na soko, hatukuwa na mipango mizuri mbaazi ilianguka sana bei na kuwavunja moyo wakulima.
Mwaka jana mbaazi iliuzwa kwa Tsh 300 kwa kilo, lakini mwaka huu wakulima wameuza kwa Tsh 2000 na zaidi kwa kilo,”ameeleza Rais Samia.
Amebainisha kuwa huo ndio mtindo Serikali utakaoendelea nao katika mazao mengine wa kumuunganisha mkulima na soko.
Ametaja hatua nyingine kuwa Serikali imejithatiti kujenga barabara kuunganisha Mikoa, Mikoa na Wilaya zake pamoja na barabara kubwa na nchi jirani ili kupata masoko ya nchi jirani.
“Tunatengeneza bandari zetu Tanzania, Bandari ya Dar es Salaam, Zanzibar, Tanga, Mtwara zote ziweze kupokea meli zinazoweza kushusha na kuchukua mazao kwenda nje,” amesema Rais.
“Pale bandarini tunajenga sehemu ambayo itaweza kuhifadhi perishable goods (mazao ambayo yanaharibika kwa haraka) yaweze kuhifadhiwa haraka yakisubiri usafiri,” ameeleza Rais.