Wakulima wa zabibu kutoka kata ya Hombolo, Dodoma wameendelea kuomba serikali kuwatafutia wawekezaji wengine ili wasiendelee kupata hasara kutokana na mazao yao kuharibika kwa kukosa soko. Wakulima hao wamesema hayo kwa Mkuu wa mkoa huo Dk. Binilith Mahenge alipotembelea mashamba hayo na kujionea uharibifu huo unaoendelea. Wakulima hao wamesema ili hali hiyo isiendelee kutokea inatakiwa kuongeza viwanda kwani wanazalisha kwa wingi.
“Tangu serikali ya awamu ya tano iseme tufanye kazi, zabibu zinazotoka nchini ni zaidi ya hizi mnazozishuhudia sasa, zaidi ya miaka mitatu tutatengeneza bomu la hatari la kukosa soko hapa”. Amesema mmoja wa wakulima hao.
Wakulima hao wameomba serikali kuangalia uwezekano wa kuleta wawekezaji zaidi katika eneo la Hombolo wakidai aliyekuwepo hivi sasa (kiwanda cha Cetawico) ana uwezo mdogo wa kununua zabibu hizo.
Baada ya kujionea hali halisi, Dk. Mahenge ametoa maagizo kwa Katibu Tawala wa mkoa huo kuwaita awekezaji wote wa viwanda pamoja na wanunuaji zabibu ili wapate nafasi ya kujadiliana na kuangalia uwezekano wa kutatua tatizo hilo.
“Pia ni vyema mkaanzisha chama cha ushirika wa zabibu kama ilivyo kwenye mazao mengine kwa kuwa mkakati uliopo ni kuinua zao hilo liwe kama mazao mengine ikiwemo kahawa”. Ameshauri Mkuu hyo wa mkoa.