Home AJIRA Mabadiliko ya kiuchumi kwa wafanyakazi yaja

Mabadiliko ya kiuchumi kwa wafanyakazi yaja

0 comment 27 views

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amewashauri wafanyakazi wote nchini kujiletea maendeleo na kusaidia katika ujenzi wa taifa kwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazowazunguka. Waziri Mhagama ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na viongozi wanawake kutoka mkoani Morogoro kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na TAMIKO, CWT, TUICO, TALGU, TULGE, TPAWU na CHODAWU.

Waziri Mhagama ameweka wazi kuwa, serikali imeweka mikakati ya kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wafanyakazi kwa kuhakikisha wanakuwa washiriki kwenye dhana ya uchumi wa viwanda ili kuwawezesha wafanyakazi nao kushiriki katika mipango ya maendeleo ya taifa.

“Mnao uwezo wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na mkawa chachu ya maendeleo ya viwanda kwenye uchumi wa taifa letu, kwa kuweza kutoa ajira, vilevile kuwasaidia ninyi kupiga hatua za maendeleo kwa kufanya kazi kwa uzalendo na weledi kwa kutumia sera ya viwanda”. Amesema Mhagama.

Mbali na hayo, Waziri huyo ameongeza kuwa sera ya uchumi wa viwanda iliyoanzishwa na Rais Magufuli inalenga kuboresha maisha ya watanzania.

“Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza azma ya kujenga Tanzania ya viwanda, hivyo nitafurahi sana kama Waziri mwenye dhamana ya wafanyakazi kuhakikisha tunaleta mabadiliko chanya ya kiuchumi kwa wafanyakazi.” Amefafanua Mhagama.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Beng’i Issa ameelezea sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inayolenga kutengeneza mazingira mazuri ya upatikanaji wa mitaji ili kuwainua wananchi.

“Wanawake wana mchango mkubwa katika jamii, hivyo ni vyema mkatumia vizuri fursa hii kwa kuanzisha shughuli zitakazowasaidia kuongeza vyanzo vya mapato na kuleta maendeleo kupitia ushirika wenu na hivyo kuwarahisishia kupata mikopo ya kuendeleza shughuli hizo.” Alisema Issa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter