Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali imeweka mkazo mkubwa katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji kuanzaia mwaka wa fedha ujao.
Akihutubia wananchi wa Mkoa wa Tabora Rais Samia alisisitiza kuwa sekta hizo zinawagusa wananchi moja kwa moja.
Alisema kilimo cha maeneo makubwa kitasaidia kuondoa uhaba wa bidhaa mbalimbali kama mafuta ya kula na kumuagiza Waziri wa Kilimo kupunguza bajeti ya matumizi ya manunuzi ya mbolea na kuelekeza fedha hizo kwenye kilimo kikubwa.
Rais Samia ametoa wito kwa watafiti wa mbegu za kilimo kufanya utafiti wa mbegu bora za kisasa ili wakulima wapate mbegu zitakazowapa mavuno mazuri.
Aidha, Rais amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhifadhi chakula kilichopo ili kitoshe kutumika kabla ya kupata mvua zingine za uhakika kwa kuwa mwaka huu wa mavuno yamekuwa haba kutokana na ukosefu wa mvua.
Hali kadhalika, Rais Samia amesema ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa mvua ambayo inaathiri kilimo, serikali inaweka mikakati ya kufanya kilimo cha umwagiliaji ambacho hakitotegemea misimu ya mvua.
Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Maafisa Tawala nchini kuhakikisha kuwa wanasimamia matumizi ya fedha zinazopelekwa katika Halmashauri zao kuhakikisha zinafanyakazi iliyokusudiwa katika kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.