Naibu Waziri wa Kilimo Omari Mgumba amesema licha cha kukumbwa na changamoto mbalimbali, zao la korosho limeingiza fedha za kigeni Sh. 1,136,609,586,722 katika kipindi kilichoishia Januari 2018. Akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Abdallah Nachuma, Naibu Waziri Mgumba amesema japokuwa mchango huo ni mkubwa ikilinganishwa na mazao mengine ya biashara, zao la korosho kwa ujumla limekuwa na changamoto ambazo serikali imekuwa ikifanya jitihada kuzitatua ikiwemo kuongeza bei ya korosho na kutafuta masoko ya uhakika.
Katika maelezo yake, Naibu Waziri amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuyumba kwa bei ya korosho katika soko la dunia, tija ndogo kwenye uzalishaji, wakulima kutotumia miche bora na vilevile matumizi hafifu ya pembejeo.
“Katika kukabiliana na changamoto hizo, serikali imeboresha mfumo wa uuzaji wa korosho kwa kuimarisha usimamizi na ukaguzi kuanzia ngazi ya vyama vya msingi, maghala makuu, maghala ya hifadhi na kutoa elimu, kurejeshwa kwa kiwanda cha BUCCO cha mkoani Lindi cha ubanguaji wa korosho, ujenzi wa maghala matatu ya kuhifadhia korosho katika mikoa ya Lindi, Pwani na Tanga ili kuongeza kiwango cha uhifadhi na ubora wa korosho pamoja na kuzalisha miche bora 10,000,000 na kuisambaza kwa wakulima bure”. Ameeleza Mgumba.