Home KILIMO Magufuli awajia juu wanaodai kutolipwa korosho

Magufuli awajia juu wanaodai kutolipwa korosho

0 comment 92 views

Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amewaonya wakulima wa korosho wanaodanganya kutolipwa fedha zao na kuagiza hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao. Rais Magufuli ameeleza hayo mkoani Mtwara wakati wa sherehe za kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege na kuwataka wakulima hao kuacha kutoa kisingizio hicho wakati serikali imeshawalipa fedha zao.

“Wakulima 17,616 hawajalipwa wenye kilo 1,500 kwa sababu nyingi tu, wapo waliowekewa fedha kwenye benki unakuta akaunti aliyoitaja jina ni tofauti na lake wapo waliokuwa hawana akaunti wakazungumza ilipiwe kwenye akaunti ya shangazi sasa fedha ya serikali haiendi hivyo. Waliotoa maelezo na wakabadilisha wakafungua akaunti na kadhalika sasa ni karibu asilimia 98 hadi 99 na ninataka niwaambie orodha yao ninayo, kila wilaya, mkoa, kijiji, akaunti na jina alilolipwa na nitamuachia Mkuu wa Mkoa ili mshirikiane na Mkuu wa Wilaya ili muangalie hao waliolipwa. Kukata mzizi wa fitina nimekuja na boksi lenye orodha ya majina ya watu waliolipwa fedha zao za korosho zilizokuwa chini ya kilo 1,500”. Amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ametoa msamaha kwa wafanyabiashara walanguzi (kangomba) na kuwataka kuacha biashara hiyo mwaka huu huku akitoa maagizo kwa wahakiki kuzihakiki korosho zao ili zinunuliwe.

“Hawa wa kangomba nawasamehe mwaka huu, maana walinunua kwa rahisi ili wakafanya nao biashara ya faida kama zinavyofanyika biashara nyingine, mfano mtu ananunua kuku wake kwa bei rahisi anakaa nae siku mbili tatu anamlisha anamuuza kwa bei ya juu, sasa na hawa nawasamehe, wakiri wanazo zihakikiwe tuzinunue, ila biashara hiyo ikome mwaka huu”. Amesema Rais Magufuli.

Mbali na hayo, pia ametoa wito kwa wafanyabiashara wadogo kutumia vitambulisho vya wajasiriamali walivyopewa ili wasipate usumbufu wowote wakati wanafanya shughuli zao.

“Itafika mahali wale ambao hawatakuwa na vitambulisho hawataruhusiwa kufanya biashara katika baadhi ya maeneo kwa hiyo tumieni fursa hiyo na mnapokuwa na vitambulisho hivyo hakuna kudaiwa na mtu yeyote”. Amesema Rais Magufuli.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter