Waziri Mkuu wa Kassim Majaliwa ametoa maagizo kwa warajisi wasaidizi wa ushirika kutoka mikoa yote inayolima korosho nchini kuandaa semina maalum kwa ajili ya maafisa ushirika, viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS), maafisa ugani na wakulima ili kuwawezesha kubaini na kupanga korosho katika madaraja kuanzia ngazi ya vyama vya msingi.
Majaliwa amesema hayo wakati alipotembelea kiwanda cha korosho cha BUKO kilichopo manispaa ya Lindi na kushuhudia korosho zikipimwa ubora kwenye ghala kuu lililopo kiwandani hapo na kueleza kuwa, kufanya hivyo kutamsaidia mkulima kufahamu korosho aliyoipeleka ina ubora gani akiwa huko kijijini na wanapoifikisha kwenye ghala kuu wafanye kazi ya kuthibitisha ili kuondoa malalamiko kuhusu madaraja .
“Zoezi hili licha ya kuthibitisha ubora itasaidia kuboresha uzalishaji kwani wakulima wataelimishwa namna ya kuimarisha na kuboresha uzalishaji wa korosho nchini ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya viatilifu“. Amesema Waziri Mkuu.
Majaliwa ameagiza semina hizo kufanyika mwakani ili baada ya kupata mafunzo hayo, maafisa ushirika wawasaidie wakulima kutambua ubora wa korosho wanazopeleka kuuza msimu ujao. Waziri Mkuu amewataka maafisa kilimo na maafisa ushirika kukutana katika semina hizo ili kupata taaluma hiyo itakayowawezesha kupima korosho na kuitenga katika madaraja na hivyo kuepuka changamoto zinazojitokeza wakati wa mauzo.