Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa hadi kufikia mwisho wa mwezi Machi, wakulima wote wa zao la korosho watakuwa wamelipwa fedha zao kwani uhakiki tayari umekamilika kwa kiasi kikubwa. Hasunga amesema hayo mkoani Lindi wakati wa mkutano na wajumbe kutoka kamati hiyo, viongozi, wataalamu pamoja na wakulima wa korosho mkoani humo.
“Kumekuwa na urasimu mkubwa tangu kuanza kwa uhakiki, lakini sasa tumeamua kama serikali kabla ya mwisho wa mwezi huu wa tatu, wakulima wote wawe wamelipwa malipo yao ili kuondoa adha wanazokumbana nazo”. Amesema Waziri huyo.
Katika maelezo yake, Hasunga amefafanua kuwa mchakato huo wa malipo unapitia hatua mbalimbali ikiwemo uhakiki, lakini amehakikisha kuwa zoezi hilo litafikia tamati hivi karibuni. Waziri huyo amesema hadi sasa, takribani tani 222,684 za korosho zimeshakusanywa na hadi kufikia mwisho wa wiki iliyopita, Sh. 596.9 bilioni kati ya Sh. 723 bilioni zinazodaiwa na wakulima tayari zimeshalipwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Dk. Christine Ishengoma amemuelekeza Waziri Hasunga kuhakikisha taarifa za malipo za wakulima wote wa korosho zinawasilishwa bungeni ifikapo Aprili 02 mwaka huu.