Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema zaidi ya Sh. 500 bilioni tayari zimeshalipwa kwa wakulima wa korosho huku malipo yakiwa bado yanaendelea kwa wakulima waliosalia. Majaliwa amesema hayo bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Zuberi Kuchauka, Mbunge wa Liwale aliyehoji kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho ambao walikuwa wakilipwa Sh. 2,600 kwa kilo wakati Rais Dk. Magufuli alitangaza kuwa serikali itanunua kilo moja ya korosho kwa Sh. 3,300.
“Malipo yanaendelea na sehemu kubwa ni kwa wakulima wenye kilo zaidi ya 1,500, serikali itanunua korosho zote kama ilivyoelezwa. Taratibu zinazofanyika ni kuhakikisha anayelipwa ni muhusika. Wananchi endeleeni kuiamini serikali yenu”. Amesema Waziri Mkuu.
Majaliwa amesema serikali inapaswa kufanya uhakiki kwa wakulima, ili kujiridhisha kama ni wakulima, hivyo mara baada ya kuhakikiwa, wakulima wote watalipwa fedha zao. Aidha, Waziri Mkuu amesema tayari ametoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kuhakikisha mchakato wa uhakiki na kuwalipa wakulima wote unamalizika hadi kufikia Februari 15 mwaka huu.