Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa ameagiza taasisi za utafiti kuandika matokeo ya tafiti zao kwa lugha ya kiswahili ili kuwapa wakulima hasa wale walio vijijini urahisi wa kuzielewa na kuzitekeleza. Bashungwa ametoa maagizo hayo jijini Arusha wakati akizundua Teknolojia ya Kilimo Hifadhi (CASI) ambayo imefadhiliwa na serikali ya Australia.
Bashungwa amesema kufuatia wakulima wengi kutokuwa na elimu,, wengi wao hawaelewi lugha ya kiingereza hivyo inakuwa ngumu kwao kwenda na wakati na tafiti mpya za kiteknolojia na za kisasa ambazo ni rafiki kwa mazingira, mfano tafiti hiyo ya CASI.
“Sasa naagiza taasisi hizi za utafiti wa kilimo zibadilike anzeni kuweka mikakati ya kubadilisha vitabu vyenu vya utafiti na kuweka katika lugha ya kiswahili ili wakulima wengi wa vijijini waelewe na kuzifanyia kazi”. Amesema Naibu Waziri huyo.
Aidha, ameshauri taasisi hizo kuwapa elimu waandishi wa habari kuhusu tafiti zao ili waweze kuandaa midahalo kwa lugha ya kiswahili huku wakiwashirikisha wakulima. Kupitia elimu hiyo, waandishi pia wanaweza kuandika habari mbalimbali kuhusu tafiti hizo ili kuwaelimisha zaidi wakulima nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa amepongeza matokeo ya teknolojia hiyo hasa kwa sababu ni rafiki kwa mazingira na inamletea faida mkulima.
“Tunachoomba itangazwe zaidi kwenye vyombo vya habari na serikali iongeze bajeti za watafiti ili wafanye kazi nzuri na kuharakisha kupeleka bungeni rasimu maandiko ya Sheria ili tutengeneze Sheria yenye tija kwa kulinda wakulima”. Amesema Mgimwa.