Na Mwandishi wetu
Usiri uliotawala mradi wa utafiti wa majaribio wa mbegu wa Water Efficient Maize for Africa (WEMA), umepelekea asasi za kiraia kutoka nchi tano barani Afrika ikiwemo Tanzania kuupinga.
Hayo yamekuja baada ya asasi hizo kutoka nchini Kenya, Uganda, Msumbiji, Tanzania na Afrika Kusini kukutana mjini Naivasha Kenya kwa siku tatu na kukubaliana kwa kauli moja kwamba teknolojia hiyo si rafiki na wadau wote duniani wanaipinga.
Majaribio haya ya mbegu za mahindi yanayoendelea katika nchi hizi tano yana lengo la kusuluhisha matatizo ya ukame,wadudu na magugu pindi utakapokamilika. Mratibu wa Tanzania Alliance for Biodivesity (Tabio) Abdallah Ramadhani Mkindi katika taarifa yake amesema, mabadiliko ya tabia ya nchi ni changamoto kwa wakulima kote Afrika na mazao kama mahindi, ngano na mpunga yanaathirika zaidi na ongezeko la joto.
Tafiti ya WEMA inaonekana kama njia ya makampuni makubwa kijimilikisha sekta ya mbegu. Wakulima wataendelea kutegemea mbegu hizi wakati makumpuni haya yakinufaika. Asasi hizo za kiraia zimesisitiza suluhisho la kudumu la mabadiliko ya tabia ya nchi lipatikane na mradi huu ufanyiwe uchunguzi wa kina zaidi.
Popote barani Afrika mradi huo ilipofanyika usiri mkubwa umetawala. Mwaka huu Burkina Faso inaendesha operesheni maalum ya kung’oa zao la pamba. Huko Ujerumani teknolojia hii imepigwa marufuku kabisa.