Na Mwandishi wetu
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imejitolea kuwapa mafunzo ya siku moja wakulima mkoani Lindi ili kuwasaidia kulima kilimo chenye manufaa zaidi. Sherehe hizi ambazo zinafanyika kitaifa mkoani humo katika uwanja wa maonyesho ya Kilimo wa Ngongo zinabeba kaulimbiu isemayo ” Zalisha kwa tija mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kufikia uchumi wa kati ” .
Hatua hii imekuja badala ya kuona kuna haja kubwa ya wakulima kujifunza kilimo cha kisayansi chenye manufaa na tija zaidi. Wakulima wengi hapa nchini wanashindwa kijiendeleza kwa sababu wanafanya kilimo cha mazoea hivyo kupata faida kidogo sana au kutokupata kabisa. Kila mwaka hapa nchini takribani hekta milioni 5.1 hulimwa. Kati ya hizo asilimia 85 ni mazao ya chakula tu. Ifahamike pia kuwa wanawake ndio wafanyakazi wakubwa mashambani. Uzalishaji wa kilimo Tanzania hutegemeana sana na mvua.
Kupitia maonyesho haya ya nane nane, wakulima na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wanashauriwa kujitokeza kwa wingi ili wapate fursa ya kujifunza mambo mengi, wapate kujitangaza kibiashara, kubadilishana mawazo na kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa kilimo.
Zaidi ya asilimia 80 ya wananchi hutegemea kilimo kama ajira yao nchini. Ardhi ya kilimo na mazao inayolimwa kwa jembe la mkono ni asilimia 70. Hivyo wananchi wengi wanajiingizia kipato na kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za kilimo. Ni asilimia 10 pekee ndiyo hulimwa kwa kutumia trekta huku asilimia 20 hutumia maksai.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imekua ikijitahidi kadri ya uwezo wao kukwamua wananchi kupunguza uduni katika mavuno yao. Katibu mkuu wa wizara hiyo Mhandisi Methew J. Mtigumwe amewaambia waandishi wa habari kuwa serikali inatambua matatizo yanayowakabili wakulima nchini ikiwepo pembejeo feki na amewasihi wakulima kuwa serikali ipo nao bega kwa bega hivyo wasikate tamaa.
Wakulima wadogo ambao ni wengi zaidi ukilinganisha na wale wakubwa watumie maonyesho haya kama darasa na jukwaa la kuboresha kilimo chao na kujifunza mambo mengi. Wasisite kuhudhuria kila mwaka kwani kwa kufanya hivyo wataelimika zaidi na kufanya kilimo chao kuwa chenye uhakika. Dk.Philbert Nyundoni, ambae ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) pia amewaeleza wakulima umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii. Amewashauri waitumie vizuri na kutafuta masoko maeneo mbalimbali ndani ya nchi ili viwanda vya ndani vizidi kuimarika. Kufanya hivyo kutasaidia wakulima hawa kupata masoko yenye uhakika na hivyo kujiinua kiuchumi na kufaidika na kilimo chao.
Serikali pia inatakiwa kuweka mkazo zaidi na kuwasaidia wakulima hapa nchini. Elimu zaidi itolewe ili wakulima waachane na kilimo cha kubahatisha na badala yake wajikite zaidi na kile cha umwagiliaji ambacho kina uhakika zaidi kwani kwa kufanya hivyo hawatategemea mvua.