Kampuni ya Mbolea ya YARA Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Uyole pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) zimeingia makubaliano yanayolenga kuwainua wakulima na kuendeleza sekta ya kilimo kwa ujumla.
Akizungumzia makubaliano hayo, Meneja Mkuu wa YARA Tanzania, William Ngeno amesema ni hatua muhimu katika kuleta mageuzi ya kilimo kwani wakulima wamekua na changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo kama vile mikopo na usambazaji wa pembejeo hivyo makubaliano hayo kwa kiasi kikubwa yataenda kutatua changamoto hizo
“Makubaliano haya ni muhimu sana kwani yatasaidia kubadili maisha ya wakulima wadogo ili waweze kufanya na kilimo chenye tija kitu ambacho YARA imekuwa ikisimamia kwa miaka mingi tangu kuanzishwa kwake Tanzania”. Amesema Ngeno.
Aidha, Mkurugenzi wa Mikopo TABD, Augustino Chacha amesema elimu juu ya afya ya udongo ina umuhimu mkubwa kwa wakulima ili kuchochea uzalishaji na kuongeza tija katika kilimo wanachofanya. Kwa upande wake, Dk. Tulole Bucheyeki kutoka taasisi ya utafiti Uyole amesema makubaliano hayo yatasaidia kutatua matatizo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwasumbua wakulima kwa muda mrefu.