Tanzania inatarajia kupokea takribani dola milioni 74 kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa ajili ya mazao na program ya kutoa suluhisho la kifedha kwa wakulima wadogo na miradi ya maendeleo vijijini ambayo inaendelea kufanyiwa kazi.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban baada ya kukutana na kufanya mazunguzo na Mkurugenzi Mkazi Mpya wa IFAD Sakphouseth Meng ambaye alifika Wizarani hapo kujitambulisha.
Amina amesema fedha hizo zitatolewa katika mzunguko wa 13 wa Mfuko huo huku akibainisha kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na IFAD katika kutekeleza progam mbalimbali ikiwemo mazao, kilimo na uvuvi.
“Pamoja na kujitambulisha wamekuja kutueleza malengo yao katika maeneo makuu matatu, ambayo ni uwezeshaji wa wanawake, vijana na lishe”, ameeleza Amina.
Aidha, aliushukuru Mfuko wa IFAD kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kilimo na uvuvi nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi Mpya IFAD Sakphouseth Meng, amesema Mfuko huo utaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali hususani katika kilimo na mazao.
Amesema IFAD kupitia miradi yake mbalimbali inayotekelezwa nchini inalenga kuinufaisha jamii hasa katika sekta ya uvuvi, miundombinu, mazao na kilimo.
“Tunapozungumzia watu, tunafanya kazi kwa ajili ya watu na tunajitahidi kuhakikisha kuwa watu wanakuwa kipaumbele chetu. Hili ndilo lengo letu kuu katika uwekezaji kwenye sekta ya uvuvi, miundombinu, mazao na kilimo. Lengo letu la mwisho daima ni kuhakikisha kuwa watu wanapiga hatua katika maisha yao na kuwaondoa kutoka kwenye umaskini”, amesistiza Meng.
Meng amesema katika programu zao, wanahakikisha kuwa wanawake wanakuwa na uwezo wa kiuchumi na wanashiriki kikamilifu katika maamuzi kwa kuzingatia mabadiliko ya kijinsia na kuwawezesha wanawake.
Ameongeza kuwa katika program hizo kuna fursa kubwa kwa vijana kushiriki katika biashara ndogo ndogo na ujasiriamali kwa kuanzisha miradi inayowahusisha, ikiwa ni pamoja na kituo cha usindikaji wa maziwa.