Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha David Lyamongi, amezindua rasmi teknolojia mpya ya CASI katika kilimo hifadhi. Teknolojia hiyo ambayo ni rafiki kwa mazingira na uoto wa asili inamuwezesha mkulima kuokoa muda wake wa kuandaa ardhi kwa kutifua ardhi na hivyo kuacha masalia ya mazao baada ya kuvuna na muda wa kupanda ukifika mkulima hupanda kwenye ardhi iliyo na rutuba. Kaimu huyo ameeleza kuwa, teknolojia hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia wakulima kujikwamua na kuondokana na umasikini.
Utafiti wa teknolojia hiyo umefanywa na kituo cha utafiti wa mbegu cha Seriani kilichopo Arusha kwa udhamini wa serikali ya Australia na Tanzania na takribani wakulima 55,000 wamenufaika kwa kutumia teknolojia hiyo.
Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa kilimo kituo cha Seriani Dk. Joseph Ndunguru amesema teknolojia hiyo ina manufaa makubwa kwa mkulima na nchi na itachangia kufikia uchumi wa viwanda kwani malighafi za viwandani zinatokana na shughuli za kilimo.
“Wakulima wengi wakitumia teknolojia hii itasaidia hata nchi yetu ambayo sasa inasisitiza suala la ujenzi wa viwanda kwani wakulima watachangia kuwezesha ufanisi wa viwanda vyetu kwani malighafi ya viwanda nyingi zinatokana katika kilimo”. Amesema Dk. Ndunguru.
Baadhi ya wakulima wamewataka wadau wa kilimo kwa kushirikiana na Halmashauri kuwahamasisha wakulima ambao wamezoea kilimo cha mazoea kutumia teknolojia hiyo ili kufaidika zaidi na kukuza uchumi wa nchi.