Na Mwandishi wetu
Wajumbe katika kamati ya elimu ya vyama vya ushirika mkoani Shinyanga wamesema sababu kubwa ya kushuka kwa thamani ya zao la pamba ambalo awali ilifahamika kama ‘dhahabu nyeupe’ ni kutowekwa mstari wa mbele kama ilivyo kwa mazao mengine ya kibiashara.
Wajumbe hao wameongeza kuwa soko la pamba linaendelea kufa hapa nchini kwa sababu ya bei yake kutowekwa wazi mapema na kupelekea wanunuzi kuwaibia wakulima kwa kuwapunja kilo. Bei ya zao hili imekuwa haieleweki na hali hiyo imepelekea wakulima wengi kuamua kuachana nalo ili wasipate hasara.
Kaimu Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga, Shose Monyo, amewataka maofisa ushirika katika kila wilaya kufufua vyama hivyo ambavyo vimeshakufa ili kuwezesha wakulima kuuza mazao yao kwa kupitia vyama hivyo kwani kwa kufanya hivyo, wakulima wanapata faida zaidi kuliko kuuza wenyewe kwa kampuni binafsi.
Monyo pia ameongezea kuwa kupitia vyama vya ushirika wakulima watapatiwa pembejeo bora. Naye Mratibu wa elimu wa vyama vya ushirika kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) tawi la Shinyanga Marco Sanka amesema kamati imeandaliwa kuangalia namna gani vyama vya ushirika vitaendelea kufanya kazi na kumkomboa mkulima pamoja na sekta ya viwanda kwa ujumla.