Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (Tari) mkoani Mbeya, Dk. Tulole Bucheyeki amesema ardhi ya Mbozi ina tindikali kati ya 4.2 na 5.7 kwenye kipimo cha PH, hali ambayo inapelekea wakulima katika eneo hilo kupoteza hadi asilimia 30 ya mazao yao kila mwaka.
“Kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakipata mazao duni sana na imefikia hatua kwamba sasa hivi mkulima anapata chini ya tani moja ya mahindi kwenye hekta moja, sababu ni nyingi moja wapo ni upungufu wa rutuba kwenye udongo, lakini sasa hivi tena tumegundua kwamba kuna tatizo la udongo umekuwa mchachu, yaani asidi imeongezeka kwenye udongo”. Amesema Dk. Bucheyeki.
Mkurugenzi huyo amesema kufuatia tatizo hilo, wameanza kuwaelekeza wakulima kutumia mbolea kama inavyotakiwa na kutibu udongo huo kwa kumwaga chokaa kwenye mashamba, jambo ambalo limeleta mafanikio kwa wakulima.
Naye Mtafiti Johnson Mtama amesema baada ya majaribio, wameanza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya chokaa ili waweze kupata mazao zaidi. Amefafanua kuwa mkulima hutakiwa kuweka mifuko 12 ya chokaa katika katika ekari moja na kutoweka tena hadi baada ya miaka minne. Baada ya kuweka chokaa hiyo mkulima anatakiwa kuwaita wataalamu kupima kiwango cha tindikali ili kupata maelekezo zaidi.