Waziri wa Kilimo Dk. Charles Tizeba amesema kuwa serikali imefikia maamuzi ya kufuta deni la zaidi ya Sh. 30 bilioni ambalo lilitokana na mkopo wa viuatilifu kwa wakulima wa zao la pamba. Dk. Tizeba amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi uliofanyika wilayani Igunga ambapo pia alipata nafasi ya kutangaza bei mpya ya pamba kuwa Sh. 1,100 kwa kilo.
Akitolea ufafanuzi uamuzi huo wa serikali, Waziri huyo amesema serikali imeamua kusamehe deni hilo ili kuwapunguzia gharama wakulima ambao hivi sasa watalipa mkopo wa mbegu pekee. Dk. Tizeba ameongeza kuwa serikali imejipanga kusambaza bure viuatilifu na kuimarisha huduma za ugani kwa wakulima katika msimu ujao wa pamba ili kuongeza tija.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba (TCB) Marco Mtunga amesema msimu huu, inatarajiwa kuwa takribani kilo milioni 600 za pamba ambazo zimelimwa na wakulima zaidi ya 500,000 kutoka mikoa 17 hapa nchini zitavunwa.