Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya soko la bidhaa ghafi, Tanzania Mercantile Exchange Plc (TMX) Godfrey Malekano amesema baada ya muda mrefu hatimaye kampuni hiyo inatarajia kuanza kazi mwezi Mei kupitia mfuko wa stakabadhi na mazao watakayoanza nayo ni pamba na ufuta.
Amesema TMX hivi sasa ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kutekeleza mfumo wa kupokea mbegu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa uzinduzi wa masoko hayo. Mbali na hayo, Malekano pia ameeleza kuwa tayari benki sita ambazo wanachama watapata nafasi ya kufungua akaunti kwa ajili ya kuuza mazao yao zimeshachaguliwa. Benki hizo za biashara ni pamoja na NMB, TIB Corporate, CRDB, Exim, Standard Chartered na Azania. Vilevile, mazao yatauzwa kupitia kampuni nne za mawakala.
Mwanzoni mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea kampuni na kuagiza kuharakishwa kwa mchakato wa kuanza kwa masoko hayo ambapo aliwataka waunde timu zenye wataalamu ambao watatembelea maeneo inayolimwa pamba.