Samadi ni aina ya mbolea ambayo hutokana na aidha mimea, wanyama waliooza au kinyesi cha wanyama kama ng’ombe, kondoo, mbuzi, kuku na wengine. Mbolea hii imezoeleka kama mbolea ya asili isiyokuwa na kemikali, na watu wengi hususani wenye hali ya chini hutumia kwa sababu inapatikana kwa gharama nafuu.
Wataalamu wa kilimo wanawashauri wakulima kuacha masalia ya mavuno yao mashambani ili baada ya muda masalia yale yakioza na kugeuka kuwa samadi, yaweze kuipa ardhi rutuba ambayo husaidia pale mkulima atakapolima tena, hivyo kuongeza uzalishaji katika mazao.
Ni vyema kufuata ushauri huo kwaniinaelezwa kuwa mbolea ya samadi huwa na chumvi, ambayo ardhi huitaji ili kukuza mazao inavyotakiwa. Kwa mfano ng’ombe 50 zina uwezo wa kutoa tani 600 kila mwaka ambapo kupitia samadi hiyo ardhi hupata kilo 3048 za chumvi chumvi za nitrate, kilo 544 za phosphate, na kilo 2722 za Potash, pamoja na kiasi kidogo cha Boron, Copper, Manganese na Zinc.
Samadi husaidia udongo kuwa katika hali nzuri, kwani uwepo wa samadi kwenye ardhi huisaidia ardhi kuhifadhi unyevu kwa muda mrefu, kushikamana vizuri, na kuongeza rutuba kwa ujumla.
Mbali na hayo, mmomonyoko wa udongo hupungua au kuisha kabisa kama kuna uwepo wa samadi katika ardhi husika. Pia inashauriwa kwa samadi zinazotokana na wanyama kutunzwa vizuri kabla hazijafika mashambani ili nguvu yake isipungue. Kwa mfano, endapo mbolea ya ng’ombe itanyeshewa na mvua basi virutubisho kama nitrate vinaweza kupungua hivyo kupunguza thamani ya mbolea hiyo.
Aidha, samadi ni moja ya njia ya kujipatia kipato hususani kwa wafugaji ambao wanaweza kuwa ni wakulima pia Ili kuhakikisha mazao yanakua vizuri na kuongeza kipato kwa mkulima ni muhimu mkulima akatumia samadi ili kupata matokea mazuri zaidi.