Wakulima wamekuwa wakihamasishwa kufanya kilimo cha umwagiliaji ili kuweza kupata faida zaidi. Wakulima wadogo wana uelewa wa aina chache za mifumo ya umwagiliaji kwa mfano mfumo wa matone, sprinkler na mfumo wa hydroponics ambao hufanyika kwenye greenhouse. Kuna aina nyingi za mifumo ya umwagiliaji kutokana na ukubwa wa shamba pamoja na aina ya kilimo kinachofanyika.
Aina nyingine za umwagiliaji ni kama umwagiliaji wa chini (surface irrigation), umwagiliaji mdogo mfano umwagiliaji wa matone (drip irrigation), umwagiliaji wa sprinkler; hapa kuna aina kadhaa ambazo ni mfumo wa center pivot, mfumo wa kusonga (lateral move-sideroll, wheel line, wheelmove) na mfumo wa hose.
Yafuatayo ni mambo kadhaa ya ambayo mkulima anatakiwa kuzingatia ili kuweza kupata mfumo sahihi wa umwagiliaji katika shamba lake.
Aina ya Udongo
Suala la udongo ni muhimu kuzingatia ili kuweza kupata mfumo sahihi wa umwagiliaji. Muundo wa udongo/mchanga huathiri uhitaji wa maji, kwa mfano udongo wa mfinyanzi hufyonza zaidi maji hivyo hauhitaji maji mengi, tofauti na mchanga wa kawaida ambao huhitaji maji mengi. Hivyo kwa kujua aina ya udongo inakuwa rahisi kwa mkulima kujua aina ya mfumo wa umwagiliaji unaohitajika.
Topografia
Hapa mkulima anatakiwa kuangalia kama shamba lake lipo mlimani, tambalale au katika bonde ili kuweza kuamua aina ya mfumo wa umwagiliaji utakaofaa. Kwa mfano ni rahisi kutumia mfumo wa matone katika sehemu tambalale au sehemu zenye milima lakini si rahisi kutumia mfumo wa sprinkler katika maeneo ya milimani kwani mazao mengine yanaweza yasipate maji ya kutosha na kupelekea mkulima kupata hasara.
Hali ya hewa
Hali ya hewa pia ina nafasi kubwa katika kumsaidia mkulima kuchagua mfumo sahihi wa umwagiliaji. Mfumo wa sprinkler sio sahihi katika sehemu zenye upepo, jua kali na joto kwani utapelekea upotevu mwingi wa maji na hii inaweza kusababisha mkulima apoteze fedha nyingi. Katika maeneo yenye joto mkulima atanufaika zaidi ikiwa atatumia mfumo wa matone ambayo huenda moja kwa moja katika mazao.
Aina ya mazao
Sio kila mazao yanahitaji umwagiliaji kutokana na uwekezaji mkubwa ambao hufanyika katika mifumo hiyo. Ni vyema kuwekeza mifumo hiyo katika kilimo cha mboga mboga, matunda na mazao mengine ya bustani kuliko kutumia mifumo hiyo katika mazao ya bidhaa kama ngano, maharage nk. Pia umwagiliaji wa matone hufaa zaidi katika mimea kama miti, mimea ya chini kama mboga na sio rafiki katika mimea inayokua kwa kukaribiana kama mpunga.
Upatikanaji wa maji
Jambo lingine muhimu ambalo litachangia kufanikiwa au kufeli kwa umwagiliaji ni chanzo cha maji na upatikanaji wake. Mahali ambapo chanzo kipo, kama vile katika mabwawa, ziwa na visima vya chini ya ardhi, itaamua aina ya pampu ya umwagiliaji ambayo inapaswa kutumika. Jambo jingine ambalo lazima lizingatiwe wakati wa kuchagua mfumo wa umwagiliaji ni kama vyanzo vya maji vina madini au kemikali ambazo zinaweza kuharibu mimea ikiwa itamwagiliwa moja kwa moja.
Gharama na faida
Kabla ya kuchagua mfumo wa umwagiliaji ni vyema kufanya makadirio ya gharama na faida za mfumo husika. Mbali na gharama za ujenzi na ufungaji peke yake, pia zingatia fedha zitakazotumika kwenye operesheni na matengenezo. Gharama hizo zinatakiwa kulinganishwa na faida ambayo mkulima anatarajia kupata.
Aidha, ni vizuri kupata mafunzo na ushauri kuhusu mifumo ya umwagiliaji kutoka kwa wataalamu wa kilimo ili kuweza kutumia mfumo sahihi na kupata matokeo mazuri zaidi. Kuna faida nyingi za kufanya kilimo cha umwagiliaji hivyo ni nafasi nzuri kwa wakulima kunufaika zaidi na kilimo chao.