Wakulima kutoka mkoani Katavi wameeleza kufurahishwa na hatua ya kuanza usambazaji wa zaidi ya tani 900 za mbolea ya mahindi na tumbaku na kudai hatua hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao hayo. Imeelezwa kuwa wakala mkuu wa kusambaza na kuuza pembejeo Yara amefungua ghala kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi tani 4,000 za mbolea katika mkoa huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo Crisencia Joseph amesema Katavi imefarijika kuhuhudia mbolea ikiingizwa kwa wingi na kuhifadhiwa ghalani ikisubiri msimu ujao kutokana na mkoa huo kukumbwa na changamoto ya kuchelewa kwa mbolea pamoja na nyingine msimu uliopita. Aidha, Kaimu huyo ametoa wito kwa wakulima kuzalisha kwa wingi msimu ujao kutokana na pembejeo kujitosheleza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wakala Mkuu wa Yara wa Nyanda za Juu, Olais Oleseenga amesema hadi kufikia sasa, takribani tani 940 za mbolea zimeshawasili mkoani Katavi ambapo tani 80 kati ya hizo zikiwa ni mbolea ya tumbaku na nyingine zikiwa za mahindi.