Meneja wa Biashara kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB), Dickson Pangamawe ametoa wito kwa wakulima kuomba mikopo katika benki hiyo ili waweze kulima kilimo chenye tija na kitakachowawezesha kupata masoko ndani na nje ya nchi. Pangamawe amesema hayo jijini Arusha wakati wa kufunga maonyesho ya taasisi za fedha zinazotoa huduma ya mikopo na kueleza kuwa, benki hiyo inatoa huduma kwa wakulima wadogo waliojiunga katika vikundi, wakulima wa kati pamoja na wakubwa kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara, Wasindikaji na Wasafirishaji wa mboga, viungo, matunda na maua nchini (TAHA).
“Natoa wito kwa wakulima wote nchini, kufikia malengo yao kupitia benki hii, waitumie kuchukua mikopo ili walime kibiashara kufikia malengo ya serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda”. Amesema Meneja huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TAHA, Erick Ng’imaryo amesema lengo ya kukutanisha taasisi za fedha na wakulima ni kutengeneza jukwaa litakaloandaa mazingira mazuri ya pande hizo mbili kujadiliana namna wakulima wanavyoweza kupata mikopo nafuu.
“Taasisi za fedha zimetenga dirisha maalum la kushughulikia kilimo kwa wakulima wadogo hadi wakubwa, sasa kazi kwenu kutumia fursa hii”. Amesema Ng’imaryo.