Home MAHOJIANO Tanzania ya kwanza kilimo cha mwani Afrika

Tanzania ya kwanza kilimo cha mwani Afrika

0 comment 245 views

Asilimia 90 ya mwani unaolimwa katika visiwa vya Zanzibar unalimwa na wanawake.

Kilimo hichi cha baharini, kimewainua wanawake wengi visiwani humo kiuchumi kutokana na biashara hiyo kukua kwa kasi.

Afisa Mawasiliano Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Bahari kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar Semeni Salum anasema kilimo hicho kimechochewa na jitihada za Rais Hussein Mwinyi katika kuchochea uchumi wa buluu.

“Kwa sasa kilimo hiki kinakua zaidi kutokana na Sera ya Rais ya uchumi wa buluu.

Wanawake wengi sasa wamejikita katika kilimo cha mwani ambapo asilimia 90 ya mwani wote unalimwa hapa Zanzibar unalimwa na wanawake katika maeneo mbalimbali ya bahari Unguja na Pemba,” anaeleza Salum.

Akizungumzia swala la mtaji kwa kilimo cha mwani, Salum anabainisha kuwa kuanzia kiasi cha Tsh 20,000 mtu anaweza kulima mwani.

“Huu mwani unalimwa baharini, hasa maeneo ya vijijini na kilimo hichi ni rahisi ambapo mahitaji makubwa ni kamba na vijiti kwa ajili ya kufunga mwani na kuuweka baharini ambapo hutumia siku 45 ndipo huvunwa,” ameeleza Salum.

Amebainisha kuwa, Tanzania ndio nchi ya kwanza kwa kilimo cha mwani Afrika ambapo asilimia 90 ya mwani huo unalimwa Zanzibar.

“Kwa dunia, Ufilipino ndio inaongoza kwa uzalishaji wa mwani, lakini hapa Afrika sisi ndio namba moja,” amesema.

Salum anaeleza kuwa kuna aina mbalimbali za mwani ikiwemo mwani wa dhahabu, kijani na zambarau.

Anasema mwani wa dhahabu unapatikana kwa urahisi sana kuliko mwani wa kijani na ule wa zambarau.

Akizungumzia faida ya zao hilo ambalo ni chakula asilia katika mwili wa binadamu anasema mwani ndio zao pekee lenye virutibisho vingi zaidi.

“Aina hizi za mwani zina virutubisho sawa isipokuwa mwani wa zambarau una uwezo mkubwa wa kuondoa sumu mwilini kuliko ule wa dhahabu na kijani,” anaeleza.

Ametaja baadhi ya faida za mwani katika mwili wa binadamu kuwa una madini ya potassium, madini muhimu katika kushusha na kudhibiti shinikizo la juu la damu (High Blood Presurre).

Nyingine ni kulainisha njia ya mfumo wa chakula, kuwezesha mmeng’enyo sahihi wa chakula, kusafisha utumbo na kutibu na kuzia vidonda vya tumbo.

Husaidia kuweka sawa kiwango cha sukari mwilini ambapo fucoxanthin katika mwani husaidia sana kuweka sawa kiwango cha sukari pamoja na kutuliza maumivu ya viungo na mifupa sababu ina viwango vya madini vya “Calcium”.

Utafiti unaonyesha kuwa watu wa nchi za Asia kama China, Japan, Korea na nyenginezo walitumia mwani kama virutubisho tiba tangu Karne ya 7.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter