Ofisa wa Biashara kutoka Benki ya Access Tanzania Limited, Prosper William, amesema benki hiyo imetoa mikopo kwa wakulima wadogo wasiopungua 6,000 ili kuendeleza sekta hiyo. William ameeleza kuwa mikopo hiyo ambayo ni kati ya Sh. 500,000 na Bilioni 1 ni mikopo ya bei nafuu zaidi sokoni na riba zake ni kati ya asilimia 10 na asilimia 16. Kwa mujibu wa Ofisa huyo, wakulima hao wataweza kulipa mikopo hiyo kipindi cha mavuno.
“Lakini mikopo imepewa kutokana na ukubwa wa biashara ya mkulima na uwezo wa kulipa kwa muda. Wakulima wengi ambao tumekuwa tukifanya nao kazi wengi ni wa kutoka mikoa ya Dar es salaam, Iringa, Shinyanga, na Tabora”. Amesema William.
Pamoja na hayo, ameeleza kuwa ili kuhakikisha mikopo hiyo inafanya kazi stahiki, benki hiyo imekuwa ikiwapa elimu wakulima hao na watu wanaojihusisha na biashara ya kilimo jinsi ya kuwekeza mikopo hiyo na kukuza biashara zao. Benki hiyo imekuwa ikishirikiana na wakulima tangu mwaka 2013 kwa lengo la kuleta maendeleo katika sekta hiyo na kuiunga mkono jitihada za serikali kwenye masuala uya kiuchumi.