Kampuni ya Apple imezindua rasmi toleo jipya la simu yake ya iPhone 11 Septemba 10 mwaka huu. Simu hiyo imezinduliwa pamoja na simu nyingine ambazo ni iPhone 11 Pro na iPhone 11 Pro Max. Jambo mojawapo la msingi linalotegemea kuwavutia wateja kununua simu hii ni bei yake kwani itauzwa kwa bei nafuu zaidi kuliko matoleo mengine ya Apple. Inaelezwa kuwa wateja wanaweza kuanza kuagiza simu hiyo kuanzia tarehe 13 Septemba mwaka huu na kuanza kutumwa kwa wateja rasmi kuanzia tarehe 20.
iPhone 11 ni toleo jipya baada ya iPhone XR, simu hii ina display ya LCD yenye inchi 6.1 ambayo kampuni ya Apple huiita “Liquid Retina HD Display” ambayo ina resolution ya 1792×828. Kama ilivyo katika iPhone XR, iPhone 11 pia hakuna 3D Touch badala yake kwenye simu hiyo kuna Haptic Touch ambayo inaweza kutumika mfumo wa iOS 13. Simu hii ipo katika muundo wa glasi ambayo Apple imeeleza kuwa ni imara zaidi kuwahi kutumika katika utengenezaji wa simu nyingine yoyote. Pia inakuja katika rangi sita tofauti ambazo ni nyeusi, nyeupe, njano, nyekundu, zambarau na kijani.
Mfumo wa kamera wa iPhone 11 umeleta utofauti mkubwa kati ya simu hiyo na XR, ambapo Apple imetambulisha kamera mpya yenye lensi mbili ambayo ni maboresho ya juu ikilinganishwa na kamera yenye lensi moja ya hapo awali. Sensor mpya za kamera hizo mbili ni (12-MP wide angle, na 12-MP Ultra wide angle) ambapo mtumiaji anaweza kupiga picha kwa upana zaidi kutokana na lensi yake yenye digrii 120.
Kitu kingine katika upande wa kamera ya mbele ni uwezo wa kupiga selfie ya polepole (slo-mo) Apple wanaiita “Slofies” ambapo kamera ina sensor ya 12MP. Kipengele kipya kilichoboreshwa katika kamera ni uwezo wa kupiga picha katika mwanga hafifu au usiku, kipengele hicho kinaitwa “Night mode”. Pia katika upande wa video mtumiaji anaweza kurekodi katika mfumo wa 4K, na mfumo huo unaweza kubadilika kutoka katika 24,30, au 60fps.
Toleo jipya la iPhone humaanisha processor mpya ya hali ya juu hivyo katika iPhone 11 kuna programu mpya iitwayo A13 Bionic. Apple imeeleza kuwa A13 ina CPU yenye spidi zaidi na GPU kwa asilimia 20 kuliko A12, ambayo tayari ilikuwa processor yenye nguvu zaidi. Katika upande wa betri, imeelezwa kuwa chaji inadumu saa moja zaidi ikilinganishwa na iPhone XR ambayo inaweza kukaa hadi masaa 17 na pia katika simu hii inawezekana kuchaji kwa haraka zaidi. Aidha, hakuna mfumo wa 5G katika toleo hili.
Apple imetoa simu hizo katika uwezo wa 64, 128 na 256 GB kwa upande wa bei 64GB itauzwa Dola za kimarekani 699 ambayo ni takribani Sh. Mil 1.6, na 128 GB itauzwa $749 sawa na Sh. Milioni 1.7 huku (256GB) kwa Dola 849 ambayo ni sawa na Sh. 1.9 milioni kwa fedha za kitanzania