Home Uncategorized Tasnia ya teknolojia kuendelea kung’aa

Tasnia ya teknolojia kuendelea kung’aa

0 comment 99 views

Zama za kidijitali zimeendelea kurahisisha upatikanaji wa taarifa hasa kutokana na maboresho ya kiteknolojia ambayo yamekuwa yakifanyika kila siku. Mbali na urahisi wa kupata taarifa, matatizo mbalimbali ya kijamii yamepatiwa ufumbuzi kutokana na teknolojia. Hii imeunda fursa kwa wajasiriamali hasa vijana kubuni na kuvumbua suluhisho mbalimbali ili kuweza kutatua changamoto na shida mbalimbali zinazoikabili jamii kwa ujumla.

Hivi sasa Barani Afrika kumekuwa na uanzilishi wa  programu mbalimbali zinazojulikana zaidi kama “Apps” ambazo zinafanya kazi kidijitali na zimelenga kusuluhisha changamoto zinazojitokeza kila siku.  Kuanzia M-Pesa, hadi uanzilishi wa programu zinazotoa ‘delivery’ ya chakula hizi zote ni mfano tosha kuwa teknolojia zinazoendeshwa kidijitali ndio zitakazokuwa zikitamba siku za mbeleni.

Katika Hafla ya 7 ya Angel Fair Africa (AFA), iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 11 mwezi huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Infotech Investment Group, Ali Mufuruki alieleza kuwa  kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza zaidi katika Elimu na Teknolojia. Ili kuweza kuwajulisha watu wengi zaidi kuhusu faida za uwekezaji katika teknolojia, Bwana Mufuruki amesema kuwa serikali inapaswa kutenga rasilimali stahiki ili kuweza kukamilisha hilo. Na kwa mashirika ya teknolojia ambayo yapo, serikali inaweza kutumia mapato kukuza mfumo endelevu wa teknolojia.

Naye , Mwenyekiti mtendaji na mwanzilishi wa Convergence Partners, Bwana Andile Ngcaba, amesema kuwa kasi ya soko katika tasnia ya teknolojia barani Afrika itaongezeka miaka 20 hadi 30 ijayo kutokana na maamuzi yanayofanyika kutokana na faida zilizopo sasa.  Licha ya kuwa na vijana wengi zaidi miaka hiyo, Ngcaba amesema kuwa inakadiliwa kuwa hadi kufika mwaka 2025, 67% ya Waafrika watakuwa na simu janja.

Aidha, Mwanzilishi wa Programu ya Nala, Benjamin Fernandez, amewashauri wajasiriamali nchini kuelekeza nguvu zaidi katika kutambua shida kuliko kutekeleza wazo.

“Utekelezaji ndio jambo la muhimu na si wazo. Kwa kuelewa shida kwanza ni rahisi kutekeleza suluhisho ipasavyo” amesema Fernandez.

Mbali na hayo, Fernandez amewashauri waanzilishi wa kampuni nchini kufanya utafiti wa kutosha kuhusu bidhaa zao na kutumia gharama kidogo kadri iwezekanavyo wakati wa kutangaza bidhaa zao-kampuni inapokuwa imeanza, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mdogo kutangaza bidhaa au huduma husika.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter