Asilimia kubwa ya watanzania hawana ufahamu wa sheria na haki zao. Jambo hili limepelekea watu wengi kutopata haki zao na kupitia wakati mgumu katika maisha. Katika upande wa sheria, watu wanaendelea kuanzisha njia mbalimbali rahisi ikiwa ni pamoja na teknolojia ili kuweza kuwaelimisha na kuwajulisha watanzania kuhusu sheria na haki zao.
Sheria Kiganjani ni programu ambayo imeanzishwa kwa dhumuni la kuwasaidia watanzania hasa waishio vijijini/mkoani katika masuala ya sheria kupitia simu ya mkononi kwa gharama nafuu.
Ni dhahiri kuwa idadi ya wananchi ni kubwa kuliko wanasheria waliopo nchini. Programu hii iliyoanzishwa Agosti, 2018 inalenga kumrahisishia mtanzania kupata huduma za kisheria kutoka kwa wanasheria waliobobea katika fani hiyo ikiwa ni pamoja na kuwasiliana kuhusu mambo mbalimbali kama maswali, kupata vidokezo nk, na kupata nyaraka na ripoti za kisheria.
Jambo lingine la kufurahisha zaidi kuhusiana na programu hii ni lugha ya mawasiliano ni Kiswahili ili kila mtu aweze kuelewa na kupata huduma husika. Pamoja na hayo, mtanzania amerahisishiwa muda na matumizi ya fedha ambapo badala ya kutumia fedha na muda mwingi kumfikia mwanasheria (wengi wanapatikana zaidi mjini) sasa unaweza kupata huduma unayohitaji katika simu yako na kulipia Sh. 2,000 tu kwa mwezi na kujipatia huduma na maelekezo zaidi kuhusu nini cha kufanya kuhusiana na changamoto zake.
Aidha mbali na huduma za kisheria, Sheria Kiganjani inatoa elimu kuhusu masuala ya kisheria, hivyo kupunguza idadi ya watu ambao hawana ufahamu wa haki zao, jambo ambalo ni zuri kwa sababu muda umefika kwa watanzania kujua haki zao.
Hadi sasa, programu hii imeshajishindia tuzo ya App bora, mwaka jana ili kujipatia mafanikio zaidi kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu zaidi hususani kwa wale waishio vijijini kwa sababu watanzania wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu sheria na umuhimu wa kutumia teknolojia kwa ajili ya manufaa yao na maendeleo yao. Elimu inaweza kutolewa kupitia mitandao ya kijamii, watu mashuhuri, maonyesho na mashindano mbalimbali ili kufikisha ujumbe kwa watanzania wengi zaidi.