Home VIWANDAMIUNDOMBINU Ghasia ahoji hatma ya maji Mtwara

Ghasia ahoji hatma ya maji Mtwara

0 comment 109 views

Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia, amehoji bungeni kuhusu mpango wa serikali katika kutekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma kuelekea Mtwara Vijijini baada ya Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa kwa kushirikiana na watendaji wake kutenga fedha kwa ajili ya mradi huo.

“Mradi ule ukitekelezwa utapeleka maji katika vijiji vya Mtwara vijijini zaidi ya 30, lakini mpaka sasa hivi huu mradi umekuwa ukisuasua na ukikutana na watendaji wanakwambia mradi upo na wakati mwingine ukikutana na Waziri anasema huu mradi haupo”. Amesema Ghasia.

Pia ameweka wazi wasiwasi wake kuhusu mradi kutekelezwa baada ya kupitia bajeti na kubaini kuwa mradi huo umetengewa kiasi cha bilioni moja ambazo hazitatosha.

“Waziri atakapokuja kutoa majibu atuambie mradi huu wa maji katika Mto Ruvuma upo au haupo? Na kama haupo sisi wa Mtwara Vijijini vile vijiji ambavyo vilipangiwa kupata maji katika mradi huu vitapelekewa maji kwa mradi gani. Hivi kweli unaweza ukatoa maji Mto Ruvuma ukafikisha Mtwara mjini kwa Sh. bilioni moja au Mh. Waziri hii ni tokeni tu, je utakuwepo? Mtaongezea fedha au bado mpo katika kusuasua uwepo au usiwepo? Ukija Waziri utupe ufafanuzi”. Amesisitiza Mbunge huyo.

Baadhi ya wabunge waliochangia hoja wameitaka serikali kutimiza wajibu wake kwa kuiongezea Wizara hiyo fedha ili iweze kufanya kazi zake ipasavyo. Pamoja na hayo, wameitaka serikali kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya kufanya utekelezaji wa miradi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter