Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amehoji kutokuwepo kwa kituo cha mabasi madogo ya umma maarufu kama daladala katika eneo la Uyole mkoani Mbeya. Rais amesema hayo aliposimamishwa na wananchi wakati wa ziara yake jijini humo.
“Yaani niwe Mbunge wa hapa nishindwe kusema hili eneo litakuwa kituo cha mabasi na watu wafanye biashara nishindwe, kwa sababu majukumu mengine ni yenu, mkikosea njia unaweza ukaenda halafu ukarudi lakini yapo mambo ukiyakosea majuto yake ni makubwa, hili nalo mnasubiri hadi Rais aje aseme”. Amesema Magufuli.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa huo, Albert Chalamila amesema kutokuwepo kwa kituo cha mabasi katika eneo hilo kumetokana na eneo lililotengwa maalum kwa ajili ya stendi na soko kumilikiwa na watu sita tofauti.
“Viwanja hivyo vilimilikishwa kwa mtu mmoja mwaka 1990 ambapo 1996 aliamua kuviuza kwa Wachina, jambo lililokuwa likifanya kutafuta namna ya kulirudisha eneo hilo kwa wananchi na baada ya kupiga hesabu ikawa kiasi cha shilingi milioni 539 kinahitajika,tukagundua kuwa fedha ni nyingi na hatuwezi kulipa. Hivyo ndani ya kikao cha baraza la madiwani wakakubaliana tumege kipande cha ardhi kutoka shule ya msingi Uyole ili tuweke stendi na soko”. Amefafanua Chalamila.