Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa, ameeleza kuwa mawasiliano ya barabara ya Morogoro-Dodoma sehemu ya maingilio ya daraja la Dumila (Daraja la Magufuli) yamerudi kama ilivyokuwa awali. Kwandikwa amesema hayo mkoani Morogoro alipofika darajani hapo kujionea athari za mvua zilizopelekea daraja hilo kubomoka na kusababisha wananchi kushindwa kutumia barabara hiyo kwa takribani masaa saba.
“Kama mlivyoshuhudia tangu asubuhi tumeanza kazi za kurudisha mawasiliano katika barabara hii, matengenezo yamekamilika na wananchi tayari wameshaanza kutumia barabara”. Amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, Kwandikwa ametoa pongezi kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kampuni ya ujenzi ya Yapi Merkezi na wadau mbalimbali waliojitokeza katika kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja kurudisha mawasiliano katika eneo hilo.
Pamoja na huyo, Naibu huyo amesema ili kuhakikisha mawasiliano ya barabara yanakuwa imara, serikali ipo katika harakati za kuandaa mpango wa kuboresha barabara hiyo ambapo kwa sasa, wataalamu wanafanya usanifu wa barabara hiyo na utakapokamilika, ujenzi utaanza mara moja.