Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo, amemuonya Mtendaji Mkuu wa wakala wa usafiri wa mabasi yaendayo kasi Dar es saalam (Dart) Mhandisi Ronald Lwakatare kufuatia kushindwa kutekeleza majukumu yake huku akimtaka kujieleza kwanini ameshidwa kumsimamia mtoa huduma, UDART. Jafo amemtaka Naibu Waziri Joseph Kakunda kufanya kikao kitakachojumuisha Mtendaji Mkuu wa Dart pamoja na mtoa huduma UDART, ili kubaini matatizo ambayo yamekuwa yakisababisha huduma hiyo kusuasua siku za hivi karibuni.
“Usafiri huu ulikuwa ni neema sana kwa wakazi wa Dar es salaam ambao wengine walikuwa wanatumia zaidi ya masaa matau kutoka Kimara kwenda Posta lakini leo hii kupitia usafiri huu wanatumia takribani dakika 40 hadi 45 hivyo hatuwezi kuacha huduma ziendelee kudorola kwa kiasi hiki”. Ameeleza Waziri huyo.
Mbali na hayo, Jafo amemuagiza Katibu Mkuu TAMISEMI Mussa Iyombe, kuendesha uchunguzi katika ofisi ya Dart ili kuona kama kuna watendaji ambao wanakwamisha huduma hiyo na kuwaondoa kisha kutoa nafasi kwa wengine watakaofanya kazi kwa ufanisi.
“Usafiri huu wa mabasi yaendayo kasi ulishalipatia heshima jiji la Dar es Salaam hadi kupata cheti cha kuwa na usafiri ulio bora na watu kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakija kujifunza kwetu juu ya mradi huu hivyo hatuwezi kuendelea kuwafumbia macho watendaji ambao hawatimizi majukumu yao”. Amesisitiza Jafo.