Misimu ya mvua hapa nchini huwa furaha kwa baadhi huku ikiwa ni changamoto kwa watu wengine. Wakulima wengi hufanya kilimo chao kwa kutegemea mvua hivyo huona kama neema pale mvua inaponyesha. Wakati huo huo, hali sio ya furaha sana kwa baadhi ya makundi ya watu kwani inamaanisha shughuli zao za kiuchumi zinakwama.
Swali la muhimu kujiuliza hapa ni kwanini miundombinu yetu haistahimili mvua? Kwanini mvua irudishe nyuma maendeleo ya baadhi ya watu? Hapa nchini hasa katika jiji la Dar es salaam watu wengi hulazimika kusitisha shughuli zao wakati wa mvua kutokana na mazingira kutokuwa rafiki kwao.
Misimu ya mvua kwa jiji la Dar es salaam inamaanisha uwepo wa foleni kubwa barabarani hali inayopelekea watu kupoteza muda mwingi katika foleni badala ya kuwa katika maeneo yao ya kazi. Mbali na uwepo wa foleni gharama za usafiri hasa bodaboda zinakuwa juu hivyo inabidi kuingia gharama kubwa kipindi chote cha mvua ukiwa unatoka nyumbani kuelekea katika eneo lako la kazi.
Mbali na kuwa na miundombinu mibovu ambayo husababisha foleni na kero kubwa kwa wananchi wakati wa mvua, pia baadhi ya wafanyabiashara hasa wadogo hupata wakati mgumu kufanya shughuli zao za kimaendeleo. Wamachinga wanaouza bidhaa zao mitaani wanakosa pa kuweka bidhaa zao na hivyo wanashindwa kujiingizia kipato. Pia wanaofanya biashara ya matunda na mbogamboga ambao hulazimika kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine wanapata wakati mgumu kufanya shughuli zao kutokana na kwamba hawana sehemu rasmi ya kuuzia bidhaa walizonazo.
Kwa wafanyabiashara wadogo walio wengi misimu ya mvua sio muda mzuri kwao kibiashara kwani faida wanayopata ni ndogo kulinganisha na wakati wa kiangazi. Japokuwa kuna maeneo maalum ambayo yametengwa na serikali kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao kama vile Machinga Complex, wengi wamekuwa wakilalamikia kodi pamoja na tozo nyingine kuwa juu hivyo hufanya biashara zao barabarani.
Mbali na misimu ya mvua kuwa kikwazo kwa baadhi ya watu kibiashara, mvua pia huja na changamoto nyingine kama magonjwa ya milipuko kutokana na mipangilio mibovu ya jiji. Sehemu nyingi mifereji hushindwa kupitisha maji ya mvua kama inavyotakiwa hivyo kusababisha maji kutwama na wananchi kuwa katika hatari ya kupata magonjwa kama kipindupindu na Malaria na hivyo kushindwa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama kawaida.
Ni kweli kuwa serikali inayo jukumu la kuhakikisha kuwa wananchi wake wanaishi katika mazingira salama yasiyo hatarishi na kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha miundombinu ya barabara, mifereji na madaraja ili yasiwe kero pindi mvua zinapoanza lakini wananchi nao wanatakiwa kutumia busara na kutumia miundombinu hiyo kistaarabu na katika njia ambayo sio haribifu kwani ni wao wenyewe wanaoishia kupata madhara kama miundombinu hii ikishindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa.