Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amegoma kuzindua stendi mpya ya mabasi makubwa ya Maili moja Kibaha mkoani Pwani kufuatia wasiwasi wa utekelezaji wa mradi huo na kusema mara baada ya uchunguzi kufanyika na kujiridhisha na mradi huo, atarudi tena kuuzindua.
“Dhumuni lililonileta ni kufungua stendi hii, tumepata malalamiko kidogo hivyo sitaweza kuifungua leo (jana) stendi hii, hivyo naomba mnipe wiki mbili au tatu nitakuja kuifungua. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni sikivu na kusikia malalamiko ya wananchi, tumepata malalamiko kidogo kuhusu stendi hii, serikali ni ya uwazi na ukweli hivyo sitofungua stendi. Naomba shughuli zote ziendelee, napenda kumpongeza sana Mkurugenzi kwa hapa mlipofikia”. Ameeleza Samia.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Kibaha, Jennifer Omolo amesema mradi huo umegharimu Sh. 3.2 bilioni. Stendi hiyo itakuwa na mabanda kumi ya kukata tiketi, mawakala 40, eneo la taxi na wafanyabiashara wadogo takribani 100.
Kwa upande wake, Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amesema ujenzi wa stendi hiyo ni wa kiwango cha juu ukilinganishwa na stendi tisa zilizopo kwenye mpango huo.
“Kwani kila kazi ina changamoto za kibinadamu, hasi na chanya, lakini wamejitahidi”. Amesema Jafo.