Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe amewataka watumiaji wa usafiri ya mabasi yaendayo kasi jijini Dar es salaam kuwa watulivu kwani serikali imejipanga kuleta mambo mazuri. Waziri huyo amesema hayo katika mkutano wa mwaka wa usafirishaji uliowakutanisha wadau wa maendeleo, sekta binafsi pamoja na mabalozi kutoka mataifa mbalimbali. Kufuatia malalamiko ya siku za hivi karibuni kutoka kwa wakazi wanaopitiwa na mradi huo, Waziri Kamwelwe amesema changamoto zilizopo hivi sasa katika mradi huo zinatokana na mchezo uliotaka kuchezwa na mwendeshaji wa mradi lakini serikali tayari imeshagundua hilo.
“Wananchi watulie mambo mazuri yanakuja watayafurahia haya yote ni matokeo ya mwendeshaji kutaka kuleta mchezo mchafu ambao serikali tukasema hapana, maana alipewa muda halafu akataka kuingia moja kwa moja na kisha atutoe kabisa. Nawaahidi kila kitu kitakuwa sawa mambo yanarekebishwa na usafiri utarudi katika hali ya kawaida na tutahakikisha kadri tunavyoendelea haya mabasi yanafika hadi uwanja wa ndege”. Amesema Waziri Kamwelwe.
Mradi huo ambao ulionekana kuwa mkombozi wa changamoto ya usafiri jijini Dar es salaam hivi sasa umekuwa ukikumbwa na adha mbalimbali ikiwemo msongamano ndani ya mabasi, hali inayofanya wananchi kukosa uhakika wa asilimia 100 wa usafiri huo.