Ujenzi wa soko la kisasa la Kisutu unatarajiwa kuanza mwezi ujao na inatarajiwa kuwa, soko hilo jipya mbali na kuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 1,500 pia litakuwa na huduma nyingine muhimu kama vile benki, maegesho ya magari, machinjio na mabucha.
Kwa mujibu wa Meya wa Manispaa ya Ilala Charles Kuyeko, Halmashauri ya Ilala imesaini mkataba na kampuni ya ujenzi ya Mohammed na kwamba kiasi cha Sh. 13.48 bilioni zimetolewa na serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo la ghorofa nne.
Kuyeko ameeleza kuwa ujenzi huo utakamilika ndani ya miezi 18 na utawasaidia wafanyabiashara wa eneo hilo kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri hasa katika misimu ya mvua.
Takribani wafanyabiashara 633 wa eneo hilo watatakiwa kuhamia eneo la Mkunguni na stendi ya zamani ya Kisutu ili kupisha ujenzi huo. Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo wamefurahishwa na ujenzi huo na kusema utawawezesha kujiongezea kipato.